Na. Julius Mtatiro;
Kujiuzulu kwa waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo pamoja na kuondolewa katika uwaziri kwa waziri wa Nyumba na Makazi Profesa Anna Tibaijuka si jambo la kuachwa lipite hivi hivi, na si jambo dogo kama tunavyodhania.
Prof Sospeter Muhongo, ni mtanzania mwenye upeo wa hali juu sana kielimu na kimaarifa. Ukianza kusoma wasifu wake huwezi kuumaliza, mara nyingi napoutizama wasifu wa Profesa Muhongo huwa naufananisha na wa Profesa Lipumba kiweledi. Tofauti yao ni kwamba mmoja ni mwanauchumi na mwingine ni mjiolojia. Lakini wote ni wasomi “nguli” kimataifa.
Profesa Muhongo alijipatia shahada ya Jiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na kisha shahada ya Uzamili (Umahiri) Chuo Kikuu cha GÓ§ttingen nchini Ujerumani na mwishowe alitunukiwa shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Berlin akibobea katika eneo hilohilo la jiolojia. Nguli huyu anasema lugha nne, Kiswahili, Kiingereza, Kijerumani na Kifaransa. Ukiongeza na lugha za kienyeji kutoka mkoa wa Mara ambao alikulia, unaweza kusema ana utajiri wa lugha.
Bahati mbaya ni kwamba, hapa duniani ukiteleza mara moja haijalishi wewe ulikuwa mwerevu kiasi gani, haijalishi wewe ulikuwa ni wa msaada kiasi gani. Mfano mdogo tu ni pale ambapo unakuta kiongozi mkubwa wa serikali ameua, sheria haibagui kama yeye ni kiongozi au la, sheria imesema tu kwamba ikiwa mtu ataua kwa makusudi atapata adhabu yake, na yule atakayeua bila kukusudia atahukumiwa kwa kiwango chake pia, sheria haijasema kuwa nani akiua aachwe na nani ahukumiwe. Haya ndiyo yamemkuta mtaalamu huyu wa miamba.
Mwezi Mei 2012, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya tano katika baraza lake baada ya kuwaondoa mawaziri sita baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini kuwa walikiuka maadili ya utumishi wa umma na kushindwa kuwajibika kisiasa kusimamia mali za umma. Katika mabadiliko hayo ya tano tangu aingie madarakani mwaka 2005, Rais Kikwete alimteua Profesa Sospeter Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini, nafasi ambayo amedumu nayo kabla ya kujiuzulu tarehe 24 Januari 2014 kutokana na kashfa ya ESCROW.
Dr. Anna Kajumulo TIBAIJUKA ni msomi wa ngazi ya shahada ya uzamivu ya sayansi ya Kilimo na Uchumi (Agro-Economics) aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi ya Kilimo cha Uppsala – Sweden. Profesa huyu ni mwanamke wa kwanza wa Kiafrika kuchaguliwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mtaifa kuongoza kushikilia wadhifa wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Makazi Duniani.
Mwanamama huyu ambaye ni Mbunge wa kuchaguliwa jimbo la Muleba – Bukoba, amefanya kazi nyingine nyingi za kimataifa na zinazoheshimika na tena ametunukiwa shahada nyingi za heshima kutokana na mchango wake katika masuala mbalimbali yanayohusina na taaluma yake. Uzoefu na wasifu wa Profesa Tibaijuka kwa Afrika na hata Tanzania, sehemu kubwa ya wanawake wasomi na wabobezi hawajaufikia na wengi wataondoka duniani bila kusogelea ngazi alizopitia mwanamama huyu machachari.
Kabla ya kujiunga Umoja wa Mataifa, Profesa Tibaijuka alikuwa mhadhiri aliyefundisha masomo ya Uchumi Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na ametunga vitabu na kuandika tafiti mbalimbali juu ya kilimo, maendeleo ya vijijini, mifumo ya ulimaji, sera za chakula, masoko ya mazao ya kilimo, jinsia na masuala ya ardhi pamoja na uchumi wa mazingira.
Baada ya kumaliza kipindi chake cha pili akitumikia umoja wa Mataifa Profesa Tibaijuka alirudi hapa nyumbani na kuingia katika kinyang’anyiro cha Ubunge kwenye jimbo la Muleba mwaka 2010 ambapo alifanikiwa kuchaguliwa na kisha Rais Kikwete alimteua kuwa waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi nafasi ambayo aliishikilia hadi tarehe 22 Disemba 2014 ambapo rais alifuta uteuzi wake wakati akilihutubia taifa kupitia wazee wa Dar Es Salaam.
Kuondoka kwa wasomi hawa wawili “nguli” katika nyadhifa kubwa kama hizi lazima kutuache tukitafakari hatima ya taifa letu. Hawa walikuwa chunguni, wakila na kunywa humo, pamoja na Waziri Mkuu, pamoja na Rais pamoja na mawaziri wengine, Je haya yaliyowaondoa ni dhambi zao peke yao na kwamba mfumo mzima wa serikali au hata ngazi zao za uteuzi zilikuwa haziyajui? Mfumo wetu wa uongozi wa maelekezo ya vimemo na ujanja kuliko hali halisi na kufuata taratibu nilidhani ungewaweka mtegoni viongozi wenye elimu ndogo na weledi wa kawaida. Kwa bahati mbaya mfumo huu unakamata hawa wenye uwezo mkubwa kitaifa na kimataifa.
Kwa mfano mama yetu “Tibaijuka” amefanya kazi Umoja wa Mataifa na anajua namna ilivyo hatari kwa viongozi kuchukua fedha zozote za mgao kutoka mahali kokote. Kama Tibaijuka angekuwa UN asingepokea zile pesa za Rugemalila na kama zingekuwa muhimu sana lazima angewauliza wenzie je akizipokea zitakuwa na madhara gani, na zaidi ya hiyo angeweza kuzipokea kwa kufuata utaratibu wa kisheria. Hapa kwetu tuna sheria ya maadili ya viongozi wa umma Na. 13 kama ilivyofanyiwa Marekebisho mwaka 2002 ambayo imeweka utaratibu wa kufuata ikiwa viongozi wanapokea zawadi au fedha.
Sheria hiyo katika kifungu cha 12 (2) (a) & (b) imeelekeza kuwa kiongozi wa umma akipokea zawadi inayozidi thamani ya shilingi 50,000 (elfu hamsini) atatakiwa kuitaja zawadi aliyopokea pamoja na thamani yake lakini kubwa kuliko yote atakabidhi zawadi hiyo kwa Afisa Mhasibu wa Ofisi inayohusika ambaye atatoa maagizo kwa maandishi kuhusu matumizi ya zawadi hiyo na jinsi ya kuishughulikia kwa njia nyingine yoyote. Ule mgao aliopewa Tibaijuka na wenzie hakuupitisha katika utaratibu wa kisheria na siyo kwamba Tibaijuka haijui sheria hii, anaijua na ni Profesa mzoefu na kiongozi wa kimataifa.
Tatizo naloliona ni kuwa, wasomi wetu hawa, maprofesa wetu hawa wanapopewa majukumu ya kujichanganya na mifumo iliyozoea rushwa “corrupted systems” nao wanaanza kucheza dansi zilezile ambazo wazoefu wa mifumo hiyo hucheza kila uchwao. Kwamba Prof. akiingia wizarani au bungeni anaweka zile nidhamu na weledi wa taaluma yake pembeni, anaanza kufuata ile tabia ya mambo yaende yawavyo “business as usual”.
Msomi mzima na yeye anaanza kucheza michezo ya kujinufaisha naye apate zaidi wakati anatambua mtu wa ngazi ya Prof. hahitaji kuiba ili aishi maana hata yule wa darasa la saba tu hahitaji kuiba ili aishi. Tofauti ya Profesa au Msomi wa ngazi ya juu na yule wa darasa la saba ni kwamba Msomi ana fursa nyingi za kujipatia kipato halali, nyingi kiasi kwamba anaweza kuzikimbia.
Msomi mzoefu ni mtu ambaye anapaswa kufanya kazi popote akiwa na msimamo thabiti na kutotishwa kwa sababu yeye hatafuti kazi ‘kazi zinamtafuta’. Kwa mfano. Prof. Muhongo hakupaswa kuingia kwenye ile michezo ya kudai fedha za ESCROW si za umma wakati jambo lenyewe lina utata mkubwa. Uhalalisho aliokuwa akiufanya ulikuwa na maana ya kuwatetea watu ambao mwisho wa siku wangemtosa na fedha wamekula wao. Muhongo ameondoka huku hajala fedha za ESCROW na aliokuwa anawatetea hivi sasa wanadai zile ni “fedha za mboga tu”, kama angelijua hili jambo na angefunuliwa kabla nadhani angeweka msimamo wa kisomi tangu tu sakata la ESCROW lilipoondolewa kwa mara ya kwanza. Lakini nafasi hiyo hana.
Kazi kubwa ya kuwachanganya wasomi nguli na wale wa kadri katika ngazi za kisiasa ina maana ya kutengeneza uongozi wa kisasa “modern leadership” unaokwenda kwa kufukuzana na viwango vya kimataifa, kuzingatia maadili, sheria, kanuni na taratibu, kwa mtizamo chanya wa maendeleo na wenye weledi ambao wananchi wakiupima wanaona, Ndiyo – huu ni uongozi unaofikiri juu ya akili zetu.
Wananchi hawawezi kuvutiwa na uongozi unaotetea wezi huku wasomi wamejaa humo uongozini, wananchi watadharau wasomi wote tu. Jumapili ijayo tutahitimisha hoja hii kwa kutoa mustakabali sahihi wa hatua ambazo wasomi wanapaswa kuchukua ili wasijikute wanatumikia mifumo iliyooza “rotten systems”.
(Julius Mtatiro ana shahada ya Uzamili (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB): +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com).
Chanzo: Gazeti la Mwananchi 08 Machi 2015 - Darubini ya Julius Sunday Mtatiro
0 comments :
Post a Comment