-->

ZIFAHAMU NYASI BANDIA PAMOJA NA MADHARA YAKE

Tanzania ni kati ya mataifa ambayo yanatumia viwanja vyenye nyasi bandia. baadhi ya viwanja vyenye nyasi ni pamoja na Uwanja wa Uhuru, Karume na Uwanja wa Azam Complex, Mbagala na Kituo cha Michezo cha JK (Dar es Salaam), Uwanja wa Gombani (Pemba) na Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.
Kwa sasa mpango ni kuuwekea nyasi bandia Uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza.
Hata hivyo, pamoja na nyasi bandia kuanza kuingia Tanzania mwaka 2008 kwa Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) kuwekewa, zimetajwa kuwa ni kati ya visababishi vya maradhi ya saratani kwa wachezaji.
Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo, mamlaka za soka Uingereza, zimetakiwa kufanyika kwa uchunguzi wa kina kuona kwamba jinsi gani hali hiyo inampata mchezaji.
Hatua ya kufanyika kwa uchunguzi ni baada ya kuwepo kwa wanamichezo wa Marekani kupimwa na kukutwa na viashiria vya saratani, na ni   kutokana na kucheza kwenye viwanja vya nyasi bandia.
Wasiwasi umeongezeka zaidi hasa baada ya kubainika kuwa mipira inayochakatwa kwa ajili ya kuwekwa viwanjani, imetokana na matairi chakavu ambayo yametengenezwa kwa kemikali za sumu kama mercury, lead, benzene na arsenic, kwa mujibu wa ripoti moja iliyotolewa hivi karibuni nchini Marekani.
Kulikuwa na hoja kwa mujibu wa familia za wamarekani ambao wachezaji wamegundulika na saratani kwamba kemikali hizo ndizo zinazochangia kugunduliwa na viashiria vya kansa na zaidi ni kwa wachezaji chipukizi na hasa magolikipa ambao hurika na kuanguka katika mipira hiyo.
Mamlaka za soka nchini Uingereza, zimetakiwa kuchunguza hayo kama kuna uwezekano wa kugundulika maradhi hayo na pia klabu kubwa duniani zinazotumia nyasi bandia, zimewasilisha taarifa baada ya kuingiwa hofu ya suala hilo baada ya kutolewa ripoti.
Mbali na viwanja vya michezo, nyasi bandia hutumika katika shule, nyumbani na maeneo ya kupumzikia.
Akiwa mwenye huzuni, June Leahy, ambaye mtoto wake wa kike alikuwa kipa wa timu ya Chuo Kikuu cha Miami, Austen Everett alifariki dunia kutokana na Lymphoma, saratani inayoharibu kinga ya mwili, alifariki akiwa na miaka 25.
Leahy anasema: “Sina shaka Austen amefariki kutokana na saratani aliyoipata uwanjani, japokuwa haipendezi kusema mchezo anaoupenda ndiyo uliomuua.
“Naziagiza mamlaka za Uingereza kuacha kutumia viwanja vya nyasi bandia hadi hapo majibu halisi ya uchunguzi yatakayopatikana kama ni salama ama la.”
Kocha wa Chuo Kikuu cha Washington, Amy Griffin, 50, mchezaji wa zamani wa timu ya taifa, alifanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa na saratani.
Anasema kuwa amefanya utafiti na kugundua kuwa wanasoka 158 walikutwa na matatizo hayo na kati ya hao, asilimia 60 walikuwa magolikipa ambao sehemu kubwa huanguka wanapochupia mipira kwenye nyasi hizo bandia.
Naye mkuu wa zamani Taasisi ya NHS, Nigel Maguire wa Marekani anaamini mtoto wake amepatikana na saratani kutokana na kucheza muda mrefu viwanja vya nyasi bandia.
Maguire aliyejiuzulu ubosi wa NHS Cumbria, mtoto wake Lewis alikuwa golikipa na wakati huo alikuwa akifanyiwa majaribio, Leeds United, kabla ya kupimwa na kugundulika na ugonjwa huo. Maguire anataka kufungiwa kwa viwanja hivyo anavyoviita 3G kwa kuwa vinasababisha matatizo.
Mipira ya matairi chakavu yaliyochakatwa, humwagwa uwanjani ili kusaidia mpira kudunda, kufyonza maji kwa urahisi wakati wa mvua na pia husaidia nyasi bandia kudumu kwa muda mrefu.
Hata hivyo, uchunguzi mwingine unasema kuwa, sumu iliyopo katika matairi chakavu kama mercury, lead, benzene, arsenic na carcinogens hufa baada ya tairi kumaliza muda wake wa matumizi.
Wasiwasi upo kwa wachezaji kwamba wanaweza kumeza mipira hiyo kwa bahati mbaya, kutumia kitu (kula) wakati akitoka mchezoni ama sumu huingia mwilini kupitia katika majeraha atakapoangua ama kugusa nyasi hizo.
Nchini Scotland, asilimia 90 ya wananchi wa Scotland hutumia nyasi bandia na kwa sasa, klabu 12 hutumia viwanja vyenye nyasi bandia, ikiwemo klabu za Ligi Kuu za Kilmarnock na  Hamilton Academical.
Nchini Scotland viwanja vya nyasi bandia hutumika kwa soka, rugby, magongo, tenisi na maeneo mengine ya michezo.
Wakati hali ikiwa hivyo, klabu nyingine ya Daraja la Kwanza ya Stenhousemuir imewasilisha barua Shirikisho la Kimataifa la Soka, Fifa pamoja na Sports and Play Construction Association (SAPCA) kutaka kujua ukweli wa afya ya wachezaji wao.
Kutokana na hali ilivyo, wanasayansi wa California nchini Marekani kwa sasa wanafanya utafiti wa tatu kuona  madhara yanayotokana na nyasi bandia.
Ni utafiti wa mamilioni ya paundi na matokeo ya utafiti huo, yanatarajiwa kutolewa baada ya miaka mwili, yaani 2018.
Wakati hayo yakiendelea hivyo, Msemaji wa Bodi ya Michezo ya Sportscotland alisisitiza kusema kuwa nyasi bandia ni salama.
Alisema: ‘Kuna kila ushahidi wa usalama kwa mipira iliyochakatwa kuwekwa katika nyasi bandia.’ Naye Msemaji wa FIFA alisema kuwa tathmini ya kitabibu pamoja na utafiti wa kina vilikwishafanyika ili kuona kama kuna tatizo la viwanja vya nyasi bandia.
Alisema: “Maelezo yalikuwa wazi, kwamba hakuna ushahidi wa moja kwa moja kama mipira ya matairi chakavu yaliyochakatwa yalikuwa na shida ama la.”
Mshauri wa Viwanja vya Nyasi bandia kutoka Kampuni ya Sports Labs Ltd, Eric O’Donnell alisema kuwa anaamini mambo yote safi na hakuna shida katika hilo. Naye kocha wa Chuo Kikuu cha Washington, Amy Griffin, 50, ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya Marekani, alifanyiwa uchunguzi baada ya kuwepo na tuhuma hizo lakini hakugundulika na tatizo.
Griffin anasema: “Nimefundisha kwa miaka 26 au 27 na katika miaka yangu 15 ya kwanza, Sikuwahi kusikia kama nyasi bandia zinashida.”
Wazalishaji wa nyasi bandia, Kampuni ya Astroturf walikanusha bidhaa zao kuwa ni hatarishi na kwamba utafiti zaidi ya 50 umefanyika na hakuna mahali inapoonyesha tatizo.
Wasemavyo madaktari wa michezo
Daktari wa timu ya Yanga, Nassor Matuzya ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari wa Michezo Tanzania (Tasma), anasema upo uwezekano kwa mwanasoka kupata saratani pindi anapocheza kwenye uwanja wenye nyasi bandia, lakini hilo linaweza kuepukika iwapo mchezaji atajiweka katika hali ya usafi.
“Vile vipira huwa na kawaida ya kutoa vumbi ambalo likikutana na jasho hugandamana kwenye vinyweleo na kuziba mfumo wa utoaji taka mwilini, hali inayoweza kuzalisha tatizo. Hili linaweza kuzuilika kama mchezaji atazingatia kanuni za afya hasa kuoga na kuwa msafi,” anasema Dk Matuzya.
Akizungumzia hali hiyo, Dk Gilbert Kigadye, daktari bingwa wa magonjwa ya wachezaji, anasema kuwa suala hilo halifahamiki rasmi na madaktari wengi wa michezo, kutokana na kutokukamilika kwa utafiti wake na jopo la madaktari wa kimataifa.
“Mpaka sasa ni ngumu kulithibitisha hilo kwa sababu ndiyo linafanyiwa utafiti na tunachokifanya sisi huku ni kungojea majibu ya huo utafiti, ” anasema Dk Kigadye.
Daktari wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Sheicky Mngazija, aliliambia gazeti hili kuwa anahitaji kujiridhisha zaidi juu ya uwezekano huo wa mchezaji kupata saratani kwenye uwanja wenye nyasi bandia.
Daktari wa timu ya Majimaji ya Songea, Shaaban Mboto anasema  tatizo hilo halijulikani duniani na bado halijafahamika na madaktari wengi wa michezo.
Nyongeza na Charles Abel
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment