Walimu Sekondari Wacheza ‘Table Tennis’ Ofisini Korogwe
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Bungu wakiwa katika ofisi za walimu kuzungumzia mafanikio na changamoto mbalimbali kitaaluma katika shule hiyo. |
Ofisi ya Walimu Shule ya Sekondari Bungu. |
Habari na Thehabari.com na HakiElimu
WANAFUNZI wa
Shule ya Sekondari Bungu iliyopo Korogwe Vijijini wamelalamikia kitendo
cha baadhi ya walimu wao kucheza mchezo wa table tennis ofisini (staff
room) tendo ambalo limekuwa likifanyika hata wakati wa kazi/vipindi vya
masomo. Malalamiko hayo yametolewa juzi ambapo mwandishi wa
Thehabari.com alitembelea shule hiyo kuangalia changamoto mbalimbali za
elimu eneo la Korogwe Vijijini.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao kiusalama na mwandishi
wa habari hizi baadhi ya wanafunzi hao walisema wapo walimu ambao
wamekuwa wakicheza mchezo huo hata wanapokuwa na vipindi jambo ambalo
huwakatisha tamaa wanafunzi. “Wapo baadhi ya walimu wamekuwa wakijisahau
na kucheza table tennis hata kama ni muda wa vipindi…na endapo
akiwaanacheza na kiongozi wa darasa asimfuate kumkumbusha kipindi
anaweza asije kabisa,” alisema mmoja wa wanafunzi hao.
Thehabari.com ilifika shuleni hapo na kuingia hadi ofisi ya walimu
(staff room) na kushuhudia meza ya table tennis ikiwa imefungwa katikati
ya ofisi hiyo tena ikipewa nafasi kubwa zaidi ya vifaa vingine vya
kikazi vya walimu hao.
Hata hivyo mwandishi wa habari hizi alipozungumza na Mkuu wa Shule ya
Sekondari Bungu,Dismas Kimweli kutaka kujua sababu ya shule hiyo kuweka
uwanja wa table tennis ofisini hapo mwalimu huyo alisema wameufunga kwa
muda kutokana na kukosa eneo la kuuweka, lakini wanafanya jitihada za
kuutoa uwanja huo.
“Ni kweli eneo hili kufungwa uwanja kama huo si sahihi…hili nalielewa
lakini tuliufunga kwa muda tu na hivi sasa tunajiandaa kuuamisha,”
alisema Kimweli. Akifafanua zaidi alisema kutofundishwa kwa baadhi ya
vipindi kwa wanafunzi hakutokani na michezo ya table tennis shuleni bali
uchache wa idadi ya walimu shuleni hapo. Alisema kutokana na uchache
huo wa walimu baadhi ya mwalimu huwa na vipindi karibia 70 kwa wiki
jambo ambalo huwazidi baadhi yao hivyo kujikuta wakitupiwa lawama.
Shule ya Sekondari Bungu iliyoanzishwa mwaka 1989 yenye jumla ya
wanafunzi 640 ina walimu 12 tu huku kati ya idadi hiyo walimu watatu kwa
wako masomoni.
Hii ni nukuu kutoka Haki Elimu
Tweets by @OmariMakoo
0 comments :
Post a Comment