HIZ UT-TAHRIR AFRIKA MASHARIKI:ZANZIBAR MSIKUBALI KAMPENI YA KUMEGWA KWA MAHAKAMA YA KAHI
Hizb ut –Tahrir Afrika Mashariki haina imani kabisa na mpango wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (GNU) kupeleka Muswada wa sheria wa kile kinachoitwa kuiboresha Mahkama ya Qadhi. Aidha, tunaonya kwa nguvu zote dhidi ya kudandiwa kwa kile kinachoitwa kuzifanyia marekebisho sheria za udhalilishaji wa kijinsia ilhali ikidhamiriwa kuasisi sheria ya suala la mgao wa mali za wanandoa baada ya kuachana (division of matrimonial assets). Jambo ambalo ni kinyume na Uislamu na kuingilia moja kwa moja mamlaka ya Mahkama ya Qadhi.
Mchakato huu wa GNU kama ilivyo michakato ya sheria nyengine na hususan kama ulivyokuwa mchakato wa kuasisiwa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2011 ni shinikizo la Madola ya nje (Gazeti la Mwananchi Juni 4, 2010. Uk 1&4). Pia unapigiwa tarumbeta na wakala wao wa ndani katika wanaoitwa wanaharakati na taasisi za kiraia zinazojinasibu na utetezi wa haki za wanawake ikiwemo Jumuiya ya wanasheria wa kike ya ZAFELA. (Zanzibar Female Lawyers)
Tunatamka wazi kwamba licha ya malengo mengine, mchakato huu umedhamiria kukimaliza kichache kilichobakia katika sheria za Kiislamu katika miamala ya ndoa, urathi na matunzo ya watoto, kumega mamlaka ya Mahkama ya Qadhi kama si kuing’owa kamwe!
Enyi Waislamu wa Zanzibar hususan Masheikh, Maimamu na Maustadhi:
Mzazi mwenye uchungu hachoshwi na ulezi wake, Sisi Hizb tunakukumbusheni tena kama tulivyokukumbusheni na kukuhadharisheni mwaka 2011 wakati harakati za kupitishwa Sheria ya Mtoto zilipopamba moto na hatimae kupitishwa. Sheria thaqili na ovu ambayo itabakisha balaa na dhima kubwa katika historia ya visiwa hivi. Jee mnajuwa kuwa pamoja na mambo mengi mabaya ya sheria ile pia imetambuwa miongoni mwa vipimo vya kunasibishwa ubaba wa mtoto ni kwa kupitia vipimo vya vijinasaba (DNA test) au hata ndoa zilizo kinyume na Uislamu? Jee hatuoni kwamba hilo litawapa uwalii na urathi wasio na haki na kuendeleza dhulma mpaka siku ya Hesabu?
Kampeni dhidi ya Mahkama ya Qadhi ni kampeni ya nje na inaendelea Kenya, Tanganyika na pia ni ajenda endelevu Zanzibar kwa kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo kuimarishwa wizara inayohusiana na masuala ya Wanawake na Watoto ili kuyaondowa majukumu hayo kwa maqadhi, kupitishwa sheria mbali mbali nk. Yote hayo hutendwa kwa kauli mbiu za ukombozi, uboreshaji, kuondowa udhalilishaji wa wanawake na watoto nk. Aidha, kwa ujanja mkubwa hupatilizwa kupitishwa sheria kama hizo wakati ambapo watu wameshughulishwa na mambo yasio na tija ikiwemo suala la katiba na mengineyo. Na vivi hivi ndivyo pia walivyopatiliza kuipitisha sheria ya Mtoto mwaka 2011 bila ya upinzani thabiti huku watu wakiwa wameshughulishwa na harakati za siasa batil za kidemokrasia.
Mwisho, Hizb inatoa mwito kwa Waislamu jumla wa Zanzibar hususan masheikh, maimamu maustadh kusimama kidete dhidi ya fitna hii na kuifedhehi waziwazi mipango na ajenda hii katika majukwaa na mimbar zetu ili kuonesha Ummah uone udhatiwa uadui uliotuzunguuka.
Aidha, tunawaonya katika wanaharakati, wanasisa na wanasheria wanaopiga debe kuingamiza Mahkama ya Qadhi kwa maslahi machache ya kidunia wazinduke na wasiendelee kujigubika guo la aibu, fedheha na uovu katika historia yao. Wao wametoka katika mifupa ya Kiislamu basi wamukhofu Mola wao wasihadaike na kichache cha kupita katika dunia hii kwa maangamizi ya kudumu milele
يَاقَوْمِ لَكُمُ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ظَاهِرِينَ فِي الأَرْضِ فَمَنْ يَنصُرُنَا مِنْ بَأْسِ اللَّهِ إِنْ جَاءَنَا َ
Enyi watu wangu! Leo mna ufalme, mmeshinda katika nchi; basi ni nani atakayetusaidia kutuokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu kama ikitufikia? ( TMQ GHAFIR 29))
Kumb: 18 / 1435 AH Ijumaa,12th Shawwal 1435 AH 08/08/2014 CE
Masoud Msellem
Naibu Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari Hizb ut Tahrir in East Africa
Simu.: +255 778 8706 09
Pepe: jukwalakhilafah@gmail.com
Hizb ut Tahrir Official Website
www.hizb-ut-tahrir.org
Hizb ut Tahrir Media Office Website
www.hizb-ut-tahrir.info
0 comments :
Post a Comment