
MWENYEKITI
wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha),
Leonce Marto amechukua fomu ya kuwania ubunge katika jimbo la Iringa
kupitia chama chake hicho.
Amechukua
fomu hiyo siku moja tu baada ya Rais Jakaya Kikwete kulihutubia na
hatimaye kulivunja bunge la 10 la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
ambalo uhai wake utakoma Agosti 20, mwaka huu.
Katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita, jimbo la Iringa Mjini limekuwa
likiongozwa na Mchungaji Peter Msigwa ambaye pia alichaguliwa kupitia
Chadema katika uchaguzi wa 2010.
Kwa
kupitia taarifa yake aliyoisambaza kupitia mitandao mbalimbali ya
kijamii jana, Marto alisema; “nawasalimu nyote wenye mapenzi mema na
Taifa letu la Tanzania na wapenda mabadiliko na demokrasia za ushindani
ndani ya vyama vya siasa kwa minajili ya katiba yetu ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 .”
“Nianze
kwa kuwashukuru watu wote ambao kwa muda wa uhai wangu wameshiriki kwa
namna moja ama nyingine kuniwezesha kufika hapa nilipo . Pili
nawashukuru viongozi , wanachama , wafuasi wa Chadema, ndugu, jamaa na
marafiki ambao kwa wingi wenu sitaweza kuwataja wote,” alisema.
Marto
alisema ameamua kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo iliyokuwa
ikiongozwa na Mchungaji Msigwa baada ya kupata msukumo wa ndani na nje
ya chama.
Alisema
kwa haraka katika fahamu zake aliona jambo hilo ni zito na la hatari
kulinganisha na watu wanavyosema kwasababu kazi ya umma ni kazi
inayohitaji dhamira safi, uadilifu, umahiri, weledi, kujali ya maisha ya
watu na maendeleo yao na zaidi sana kupenda na kutathmini Taifa na watu
wake.
Marto
alisema ilimchukua muda kujiridhisha pasipo shaka na jambo hilo kama
anaweza kubeba wito huo wa kuwatumikia wananchi wa Iringa Mjini.
“Baada
ya kutafakari kwa kina nilijipa mtihani wa kwanza wa kuzunguka nchi
yetu na kukutana na jamii za watanzania. Kwa mantiki hiyo ninayafahamu
kwa undani na kwa uhalisia wake maswala na matatizo muhimu
yanayowakabili watanzania na wana Iringa Mjini,”alisema.
Marto
alisema kwa kuwa anakidhi vigezo vya kikatiba, na kwa kuwa anaamini
Mungu amempa karama ya uongozi ambayo watu wameiona na kumuomba agombee
ubunge na kwa kuwa anayajua matatizo yanayowakabili watanzania na wana
Iringa anayajua na yamemchosha kama yalivyowachosha watanzania wengine:
Na
kwa kuwa Chadema kimejengwa kwenye mhimili na msingi mkuu wa Demokrasia
pamoja na itikadi na falsafa yake ya Nguvu ya Umma na kwa kuwa anaamini
viongozi bora wanapatikana kwa ushindani, kwa ujasiri wote aliopewa na
Mwenyezi Mungu anatangaza rasmi kuomba ridhaa ya chama chake kugombea
ubunge katika jimbo hilo.
0 comments :
Post a Comment