
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ni muungano wa hiyari “coalition of the willing” ambao ulianzishwa wakati wa Bunge Maalum la Katiba kwa lengo la kutetea katiba ya wananchi. Muda mfupi tangu kuanzishwa kwake viongozi wa vyama vilivyounda umoja huo kwenye Bunge Maalum la Katiba na wanachama wa vyama hivyo ambao walikuwa wajumbe wa BMK, waliamua kujiondoa kwenye mchakato wa Katiba Mpya baada ya kuona hawawezi kuvumilia uburuzwaji uliokuwa ukifanyika na hasa baada ya BKM kuhama kwenye mjadala wa rasimu ya katiba iliyoletwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuanza kujadili “maoni na matakwa ya Chama Cha Mapinduzi – CCM”. Mimi nilikuwa mmoja wa wanachama wa vyama hivi muhimu ambaye hadi leo naamini kuwa uamuzi wetu wa kususa BMK ulikuwa sahihi sana na utafanya historia isituhukumu.
Mara baada ya kuondoka kwenye BMK, vyama vya CUF, CHADEMA, NCCR na NLD viliamua kuanzisha ushirikiano mkubwa zaidi ili uvipeleke kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 vikiwa na nguvu kubwa na muunganiko kwenye ladha na taswira yenye uwezo wa kukiondoa chama kama CCM madarakan. Wananchi walipongeza sana uamuzi wa UKAWA na uliungwa mkono nchi nzima.
Tulishuhudia viongozi wakisaini makubaliano muhimu pale Jangwani na mchakato wa kuanza kugawana nafasi za kuwawakilisha wananchi (urais, ubunge na udiwani) kimkakati ukaanza, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa CCM inapata ushindani mkubwa zaidi kwenye uchaguzi wa mwaka huu 2015 na hasa kuishinda. Baadaye viongozi wa UKAWA waliujuliusha umma kwamba tayari mgawanyo wa majimbo umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na kwamba kilichobaki ni kufanya makubaliano ya mwisho.
Wakati wananchi wakisubiria majimbo yatangazwe na labda mgombea urais wa umoja huo atangazwe n.k. mmoja wa viongozi wa UKAWA alisikika akitoa maoni yake hadharani kwenye kikao cha juu cha chama chake akikiasa moja ya vyama vinavyounda umoja huo “kisivimbe kichwa” (tafsiri yangu) kwani “umoja ukikwama chama hicho kitagaragazwa na CCM bila huruma”. (maneno yangu).
Kauli ile haikuwa matusi kwa chama kilichopewa ujumbe na haikuwa na shida yoyote ile kwangu zaidi ya kuanza kuona kuwa kuna “bundi” amevamia umoja huo muhimu sana kwa watanzania. Kwa uzoefu wangu kama Katibu wa UKAWA kwenye Bunge Maalum la Katiba, sikuwahi kutarajia kuona viongozi wa UKAWA wakiasana hadharani, nasaa zile zilileta mashaka kwa wananchi waliosikia maneno yale na kwa wachambuzi wanajua maneno yale yangeweza kutafsiriwa vibaya na chama kilichotuhumiwa na kwamba mahali pake palikuwa ni kwenye vikao vya ndani vya UKAWA yenyewe. Lengo la makala hii si kuchambua kauli moja moja ya kiongozi wa UKAWA bali ni kujenga msingi wa matizamio ya watanzania juu ya umoja huo.
Hakika, watanzania wanaona kuwa CCM inawachelewesha kwenye mabadiliko na wangependa labda kuyapata nje ya CCM ambako kwa mtizamo wangu ni UKAWA. UKAWA inapaswa kuendelea kuwa imara hadi itakapofikia malengo yake makuu. Taarifa ambazo zinaandikwa na vyombo mbalimbali vya habari hivi sasa zikitishia kuwa huwenda umoja huo unalegalega kwenye dakika hizi za mwisho (japo hazithibitishwi na viongozi wa UKAWA) si taarifa njema sana kuzisikia masikioni. Kwa watu wanaopenda mabadiliko wangependa kusikia UKAWA ikitoka hadharani na kuwatangazia mgombea mmoja wa urais, wabunge kwa kila jimbo na diwani mmoja kwa kila kata, na si vinginevyo. Wapenda mabadiliko wasingependa kusikia tetesi za UKAWA kuyumba kwa sababu wengi wanaamini UKAWA inaundwa na viongozi weledi na wanaotizama mbali sana.
Kwa maoni yangu, UKAWA imeshateka roho na mioyo ya watanzania na wako tayari kuipatia mamlaka makubwa ndani ya nchi kuliko ilivyowahi kuwa wakati wowote katika historia ya nchi yetu. Kama wananchi wako tayari kiasi hicho ina maana wanaosubiriwa ni viongozi wa UKAWA kupokea Baraka za wananchi na kupewa ushindi mkubwa kwenye uchaguzi wa mwaka huu. La! Kama kuna kinyume na matakwa haya ya wananchi itakuwa na maana moja tu “usaliti”.
Nataka kurudia kusema kuwa, ikiwa UKAWA itashindwa kufikia malengo yake mwaka huu, ikiwa itaishindwa kuweka mgombea urais mmoja, mgombea ubunge mmoja na mgombea udiwani mmoja, huo ni usaliti mkubwa sana kwa watanzania na sina namna nyingine ya kuita kitendo hicho. Kwa msisitizo nataka kusema kuwa hilo likitokea lina maana ya moja kwa moja kuwa vyama vya CHADEMA, CUF, NCCR na NLD vitakuwa vimewasaliti watanzania ambao tayari walikuwa wameunganishwa vilivyo kusimamia mabadiliko makubwa, kazi ambayo wananchi waliianza kwenye serikali za mitaa kwa kuvipatia vyama hivyo ushindi wa asilimia zaidi ya 30 tofauti na mwaka 2009 ambapo vyama vyote hivi vilishinda chini ya asilimia 10 ya serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
Huu ndio mwaka ambao watanzania wameusubiri sana, mwaka ambao kura za wananchi zitaamua kuleta mlingano wa siasa katika nchi, utajenga kuheshimika kwa vyama vya upinzani na utaimarisha demokrasia na utawala bora. Tukumbuke kuwa, upinzani dhaifu hauwasaidii wananchi, upinzani dhaifu na uliogawanyika ndiyo unafanya serikali zilizoko madarakani zitende kinyume na matakwa ya wananchi, ziibe fedha za wananchi na zifanye kila upuuzi. Nchi yoyote yenye upinzani imara na ulioungana haiibiwi fedha zake zikatunzwa nje na watu wachache, raia wake hawateswi na kunyanyaswa bila sababu na serikali yake haina namna zaidi ya kuwajibika kwa raia kwa sababu kufanya kinyume na hapo ni kukaribisha kuondolewa madarakani.
Naamini kuwa UKAWA ina viongozi thabiti na haitayumba, na nasema kwa msisitizo kuwa ikitokea inayumba itakuwa ni “usaliti” wa demokrasia katika nchi yetu na kwa watanzania. Tusisahau kuwa, “…kama watanzania watayakosa mabadiliko kwenye vyama vya upinzani, wataendelea kuyasaka hukohuko ndani ya CCM” na tusije kuwalaumu. Na nataka kuonya kuwa, kama itatokea UKAWA inavurugika na kushindwa kutumia uchaguzi wa mwaka huu kupata ushindi mkubwa, tunaweza kusubiri miaka mingine 20 au 30 ili kufanikiwa kurejesha imani ya watanzania kwa vyama vya upinzani.
(Julius Mtatiro ni mmoja wa waasisi wa UKAWA na Katibu wa UKAWA katika Bunge Maalum la Katiba: +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com - Haya ni maoni binafsi ya mwandishi).
NOTE; Makala hii imechapishwa katika "Darubini ya Mtatiro" kwenye gazeti la Mwananchi Communications Ltd la Jumapili, 12 Julai 2015.
0 comments :
Post a Comment