“NAJUTA
kuzaliwa, sikujua kama maisha yangu yangebadilika kuwa katika hali hii!
Mke amenikimbia, jamii imenitenga, sina rafiki, ndugu nao hawanipendi.
Haya yote yananikuta kwa sababu ya huu ugonjwa ambao sikuuomba,” ndivyo
alivyoanza kusema huku akilia, Seleman Juma (pichani).
Seleman
mwenye miaka 38 na mkazi wa Vingunguti jijini Dar amekimbiwa na familia
yake kutokana na ugonjwa wa Matende unaomsumbua na amejikuta akiishi
peke yake katika mazingira yasiyostahili binadamu kuishi.
HISTORIA FUPI YA MAISHA YAKE
“Mimi ni mtoto wa tatu kati ya
wanne, katika familia yetu. Tulizaliwa Kijiji cha Masimba wilayani
Kisarawe, Pwani, nimebaki na mama baada ya baba kufariki dunia mwaka
2010.
“Sina elimu yoyote, kwani sijawahi kwenda shule hata chekechea, naamini wazazi wangu walichangia.
“Mwaka 1997, kutokana na
ugumu wa maisha niliamua kuja jijini Dar kutafuta, nikawa nafanya
kibarua katika Machinjio ya Vingunguti
“Mwaka 1999 nilimuoa Aisha
Salum. Mwaka 2002 akajifungua mtoto wetu wa kwanza, tukampa jina la
Sikujua. Kwa bahati mbaya alifariki dunia. Hapa naomba ieleweke kwamba
mpaka wakati huo sikuwa na tatizo hili la mguu.
“Mwaka 2005 Mungu akatupa
mtoto mwingine, tukampa jina la Mwajuma. Wakati huo nilikuwa naendelea
na shuguli zangu za machinjioni na nilikuwa nikiishi kwa mapenzi makubwa
na familia yangu kule Vingunguti.
TATIZO LAANZA
“Mwaka 2008 katika hali ambayo
sikuitarajia, mguu wangu wa kulia ulianza kuuma na kuvimba. Nilishangaa
ingawa si kwa kiwango cha kufikiria hali hii, baadaye kwenye uvimbe
kulipasuka na kutoa usaha mwingi na harufu kali.
“Niliamua kwenda Hospitali ya
Amana kisha Muhimbili bila mafanikio, madaktari waliniambia huenda
nilikuwa na tatizo la tende. Mguu uliendelea kutoa harufu kali sana,
hata mimi nilitamani usiwe wangu.
WAPANGAJI WAMTENGA, WAOMBA AFUKUZWE
“Niliumia zaidi baada ya
kubaini kwamba wapangaji wenzangu walianza kumlalamikia mwenye nyumba na
kutishia kuhama kama hatanifukuza mimi,” Seleman alianza kulia hapo
akidai kuwa akikumbuka anaumia sana.
“Mwenye nyumba ingawa alikuwa ananipenda lakini ilimbidi aniambie ukweli kwamba nitafute pa kuelekea.
“Siku ananiambia zilibaki
siku tatu kodi ya nyumba iishe, kwa hakika hakuna aliyenipenda kutokana
na harufu ya huu mguu. Kuna wakati hata mke wangu alikuwa akinichukia.
“Ni binti yangu pekee ndiye
aliyekuwa akinipenda, mke wangu alifika mahali akawa hataki tulale
kitanda kimoja, alinishusha chini akidai nanuka. Ilibidi nifanye hivyo.
MKE AINGIA MITINI
“Siku moja mke wangu
akaniambia kuwa amepata chumba kule Yombo, akashauri tukaishi huko. Mimi
nilikuwa nina watu nawadai kama shilingi laki tatu (300,000/-),
nilitafuta pikipiki ili kwenda kudai fedha hizo ili nimpe mke wangu
akalipie hicho chumba.
“Niliporudi jioni sikumkuta,
alichukua kila kitu kisha akatoweka na mwanangu. Niliumia sana na
nilichanganyikiwa. Nilimpigia simu na kumuuliza nini kilimpata,
akaniambia mkataba wa kuishi na mimi uliishia pale, akakata simu na
kuanzia hapo ikawa hapatikani tena.
AMFUATA MDOGO WAKE LAKINI NAKO...
“Niliondoka kwenda kwa mdogo
wangu hapahapa Vingunguti, nilikuta begi langu na baadhi ya nguo. Ina
maana kwamba mke wangu alipotoka nyumbani aliamua kupeleka mizigo yangu
kwa huyo mdogo wangu. Sawa lakini, Mungu yupo na dunia ni hiihii tu
hakuna nyingine.
“Basi, mdogo wangu alinionea
huruma sana, akaniambia niendelee kuishi naye wala nisiwe na wasiwasi.
Nilifarijika kwa kauli yake hiyo, niliishi pale kwa muda wa miezi
miwili, mguu nao ukazidi kuwa mbaya, harufu ikawa inazidi.
“Pale kwa mdogo wangu napo likazuka balaa tena! Wapangaji wenzake walikuja juu, walitishia kuhama kama sitaondoka.
Mwenye nyumba akaniambia
nitafute pa kwenda kwa sababu nataka kumfukuzia wapangaji wake. Ilibidi
nimwambie mdogo wangu, naye akaenda kwa mwenye nyumba kumwomba niendelee
kuishi.
MWENYE NYUMBA AMTIMUA
“Hata hivyo, mwenye nyumba
alikataa katakata na kumwambia mdogo wangu kama anashindwa kunifukuza
tuhame wote. Ilinibidi niondoke ili kuepuka mengi, sikujua pa kwenda,
sikuwa na fedha hata ya kupangishia chumba.
“Akili ya harakaharaka
iliniambia niende machinjioni nilikokuwa nafanyia kazi, nikawa nalala
nje, niliofanya nao kazi walinionea huruma lakini kutokana na hali yangu
ya kutoa harufu hakuna aliyekuwa tayari kunipeleka kwake.
“Lakini nawashukuru kwani
walikuwa wakininunulia chakula na kunipa fedha kidogo kwa ajili ya
kulipia bafu nioge. Lakini hapo kwenye bafu napo ikawa balaa, baadhi ya
wateja walikuwa hawataki nioge pale wakidai harufu ni kali na kwamba
nitawaambukiza ugonjwa wangu.
YALIPO MAISHA YAKE
“Kwa sasa bado naishi hapahapa
machinjioni, kuna ndoo nimepewa, nanunua maji kisha naoga nje usiku.
Kwa sasa hali yangu imezidi kuwa mbaya, ndugu na marafiki wanazidi
kunipotea, harufu inazidi, mvua ikinyesha nikijikinga upenuni mwa nyumba
za watu, wananifukuza wakidai kwamba harufu inaingia ndani.
“Kuna siku nilipata chumba,
nikawa nalala sakafuni kwani mke wangu aliondoka na kila kitu, lakini
pamoja na kulipa kodi ya chumba, muda ulipoisha mwenye nyumba
alinirudishia fedha zingine na kunitaka nitafute pa kwenda kutokana na
kero ya harufu.
“Sasa sina pa kwenda, niko
hapahapa machinjioni katika shida ya mbu na mvua. Nikisema niende
hospitali kwenye daladala, makonda wananizuia kupanda kwa vile nanuka
eti nitawafukuzia abiria. Hospitali siku zile waliniambia ugonjwa wangu
unaweza kutibika nchini India, sina uwezo wa kwenda huko, Watanzania
naombeni msaada wenu nikatibiwe.
ANACHOOMBA
“Akijitokeza msamaria mwema akanipa shilingi laki nne (400,000) nikapange chumba cha kuishi nitamshukuru sana.
“Pia naomba nguo, chakula na kama kuna uwezekano nisaidiwe kujengewa hata vyumba viwili kwa vile nina kiwanja huko Chanika.
Kwa yeyote aliyeguswa na
mateso ya Mtanzania huyu anaweza kumsaidia kwa kupitia namba yake ya
simu 0713 746572 au kupitia kwa mwandishi wa habari hii, 0768 454656 au
0783 454656.
CHANZO:MATUKIO NA VIJANA
0 comments :
Post a Comment