-->

KAMA HAUKUPATA NAFASI YA KUSOMA MAKALA YA DR KILA MKUMBO,HII HAPA BOFYA MARA MOJA KUISOMA


Dr.Kitila Mkumbo atoa dozi kwa wanasiasa,asisitiza umuhimu wa chama kuwa na. Falsafa na Itikadi.
"NIMELAZIMIKA kuendelea na mada
yangu leo kwa sababu ya msukumo wa
wasomaji walionitumia maoni.
Ninashukuru kwamba safari hii maoni
yamekuwa chanya. Sio kwamba
wasomaji wote walikubaliana na
maudhui yangu. La hasha. Nasema ni
maoni chanya kwa sababu, hata kama
baadhi ya wasomaji walinipinga,
walifanya hivyo kihoja na kwa hoja,
badala ya kejeli, mipasho na matusi.
Huu ndio utamaduni tunaotaka
kuujenga katika siasa za nchi yetu.
Utamaduni utakaojikita katika
kupingana na/au kukubaliana kihoja.
Tunataka pia vyama vya siasa
vipingane kwa hoja na katika maswala,
badala ya kupinga sura za wanasiasa.
Ndio maana mimi ni miongoni mwa
wananchi walioshangazwa,
kushtushwa na kukasirishwa na tukio
la washabiki wa CHADEMA huko
Mbeya cha kubeba jeneza wakiigiza
kubeba mwili wa moja ya wanasiasa
wasiompenda, Zitto Kabwe. Hiki
kilikuwa ni kitendo cha kihuni na
kijinga. Wanachama na washabiki wa
vyama watapata mhemuko katika
harakati za kisiasa na wanaweza
wakajikuta wanafanya mambo ya
hovyo na ya aibu, lakini ni jukumu la
viongozi wao kuonyesha uongozi na
kuhakikisha kuwa, sio tu wanakemea
matukio kama hayo, lakini wanazuia
yasitokee. Tunapoona viongozi
wananyamazia, au kuyakemea kwa
sauti isiyosikika au hata kushabikia
matukio ya kijinga kama haya inatia
shaka juu ya uwezo wao wa kiungozi.
Katika makala ya leo naeleza kidogo
aina ya chama ambacho tungependa
kichukue mbadala ya CCM na
CHADEMA katika muktadha wa itikadi
na falsafa. Itikadi na falsafa ndio
mwongozo wa chama cha siasa ndani
na nje ya serikali. Nje ya serikali itikadi
na falsafa huongoza chama katika
kuibua sera mbadala na kupinga na
kukosoa sera za chama kilichopo
madarakani. Chama cha siasa
kinapopata fursa ya kuunda serikali,
itikadi na falsafa ndio huwa dira ya
kutengeneza sera za serikali na sheria
mbalimbali katika nchi. Ndiyo kusema,
chama kisicho na itikadi na falsafa ni
sawa na debe tupu ambalo
litapeperushwa kwenda upande
wowote pale upepo utakapovuma.
Chama cha TANU na baadaye CCM
kiliundwa katika msingi thabiti wa
itikadi na falsafa. Ujamaa ndio ulikuwa
msingi wa kiitikadi na Azimio la Arusha
ilikuwa ni falsafa iliyobuniwa
kutekeleza itikadi hiyo. Pamoja na
matatizo yake kiutekelezaji, kama
anavyoanisha mwandishi William
Edgett Smith katika kitabu chake cha
‘Nyerere of Tanzania: The first decade
1961-1971, Azimio la Arusha lilikuwa
ni dira muhimu ya kifalsafa katika nchi
iliyotokana na viongozi wa kizalendo na
ambalo halikusukumwa kutoka
magharibi.
Baada ya kuachana na Azimio la
Arusha, Chama cha Mapinduzi
kimeshindwa hadi leo kuibuka na
falsafa mbadala. Badala yake
kimejikuta kikidandia sera za
magharibina mashariki ya mbali. Kwa
mfano, mwaka 2003 wakati wa awamu
ya tatu ya utawala wa Rais Benjamin
Mkapa serikali ya CCM iliibuka na
mtaalamu wa kurasimisha biashara
zisizo rasmi, Profesa Hernando de
Soto. Mtaalamu huyu akaishawishi
serikali ya Mkapa kwamba
kurasimisha biashara zisizo rasmi
kama vile mama ntilie, saluni za
nywele, uchuuzi barabarani, n.k. ndio
ilikuwa dawa ya umaskini. Ndio
ulikuwa mwanzo wa sera ya
MKURABITA. Hadi leo hatujui mafanikio
yake yaliishia wapi. Hii ilikuja wakati
serikali ikitekeleza mpango wa kukuza
uchumi na kupungza umaskini
(MKUKUTA) ambao nao ulinakiliwa
kwa kiasi kikubwa kutoka magharibi.
Leo serikali ya CCM inatekeleza
mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
(BRN) ulionakiliwa kutoka Malaysia na
tunaambiwa mpango huu ndio kiboko
ya umasikini na matatizo mengine hapa
nchini. CCM haina tena uwezo wa
kubuni falsafa za maendeleo na badala
yake inadandia sera za mataifa ya nje
ambayo mazingira ya utekelezaji ni
tofauti kabisa na hapa kwetu na ni
sababu mojawapo kwa nini sera hizi
zinagonga mwamba kila mara.
Kupoteza kwa mwelekeo kwa CCM ni
jambo ambalo Katibu Mkuu wa zamani
wa chama hicho, marehemu Horace
Kolimba, aliliona mapema miaka ya
tisini, pale alipotamka kinagaubaga
kwamba CCM imepoteza dira. Kwa
kuwa wakati huo kukosoa CCM ilikuwa
ni sawa na kumchungulia mama mkwe,
Kolimba alisakamwa na kuzodolewa
sana. Lakini leo tunaona bayana kile
ambacho alikisema Kolimba zaidi ya
miaka ishirini iliyopita.
Chama cha siasa bila itikadi na falsafa
ya kueleweka kitaishia kupigania
madaraka pekee na mara kipatapo
madaraka kitakuwa hakijui kifanye nini
na madaraka hayo, zaidi ya viongozi
wake kujinufaisha nayo kibinafsi.
Nilipojiunga CHADEMA mwaka 2005
nilikuwa na matumaini makubwa ya
kuchangia katika kujenga chama
kitakachoibuka na itikadi na falsafa
mbadala na kuziba ombwe lilioachwa
na CCM. Nimewaambia marafiki zangu
mara nyingi kwamba sikujiunga na
CHADEMA kwa sababu ya imani
kwamba kilikuwa chama bora na
ambacho nilikubaliana na misingi yake
mia kwa mia. La hasha. Nilijiunga
CHADEMA kwa sababu niliamini
kwamba kwa uchanga na uchangamfu
wake wakati huo nilikuwa na fursa ya
kutoa mchango wangu katika kukijenga
chama hiki kiwe mbadala katika nyanja
za kiitikadi, kifalsafa na kisera. Na
nilitoka CCM baada ya kujiridhisha pasi
shaka kwamba chama hiki kilikuwa
hakiwezekani tena kubadilika kutokana
na ukweli kwamba kimefikia hatua ya
usuguna hakiwezi tena kubadilika
kikiwa bado kina serikali.
Mara baada ya kujiunga, nilipata fursa
ya kukarabati itikadi na falsafa ya
CHADEMA katika hatua mbili. Kwanza,
wakati wa marekebisho ya katiba ya
chama hicho mwaka 2006 ambapo
tulifanikiwa kuitoa CHADEMA kutoka
mlengo wa kulia hadi mlengo wa kati.
Kimsingi tulikihamisha chama angalau
kidogo kutoka kwenye ubwanyenye na
kukiweka katikati pasipo ubwanyenye
wala ujamaa. Kwa lugha rahisi Katiba
ya CHADEMA ya mwaka 2006
ililazimisha CHADEMA kuachana na
ubepari kwa kiasi fulani.
Lakini fursa muhimu zaidi niliyoipata ni
mwaka 2009 kuelekea uchaguzi wa
mwaka 2010 nilipoteuliwa kuratibu
maandalizi ya ilani ya uchaguzi wa
mwaka 2010. Kwa kutumia fursa hii
mimi na wenzangu katika timu ya
kutengeneza ilani tuliifanya ukarabati
mkubwa sana kwenye msimamo wa
CHADEMA kiitikadi na kifalsafa.
Tulikihamisha chama rasmi kutoka
mlengo wa kati hadi mlengo wa kati
kushoto. Ni kwa sababu hii CHADEMA
kwa mara ya kwanza ikaweza kuhubiri
habari za kutoa elimu bure na serikali
kujiingiza moja kwa moja katika
kusimamia sekta muhimu kama vile
kilimo. Kwa kifupi kupitia ilani ya
mwaka 2010, CHADEMA kilichukua
rasmi nafasi ya CCM ya Nyerere. Na
hili liliwezekana kwa sababu CCM
yenyewe ilishakimbilia kulia
ikikumbatia ubwanyenye.
Mtu pekee aliyeshtukia ukarabati
mkubwa wa kiitikadi na kifalsafa ndani
ya chama ni Mzee Edwin Mtei. Ilikuwa
ni katika Mkutano Mkuu wa Chama wa
mwaka 2010 ambapo mzee Mtei
aliniita pembeni na kwa ukali kidogo
akaniambia kwa Kiingereza, ninanukuu:
Kitila, you have put things in the
manifesto which made me walk out of
CCM (Kitila, umeweka mambo katika
ilani ambayo yalinifanya mimi nitoke
CCM). Nikamuulize yapi hayo mzee,
akanieleza sera kama vile za elimu
bure, serikali kusimamia kilimo, na
akanionyesha sura kama mbili hivi
katika ilani ambazo kwa maoni yake,
na kweli ndivyo ilivyokuwa, zilikuwa
haziendani na msimamo wa CHADEMA
kiitikadi na kifalsafa. Nikacheka sana,
na kisha nikamwambia Mzee
umechelewa, hapa tupo kwenye
Mkutano Mkuu. Ulipaswa kutoa maoni
yako mapema ili turekebishe.
Nayaeleza haya ili wasomaji wapate
kuelewa kwamba tulikuwa
tumedhamiria kwa dhati kabisa kujenga
chama chenye misingi ya kifalsafa na
kisera inayoendana na matakwa ya
jamii yetu. Kwa kifupi tulikuwa
tumedhamiria kurudisha unyerere
kupitia CHADEMA baada ya CCM
kuutelekeza. Na kama ni usaliti huu
ndio hasa ulikuwa usaliti na tulipaswa
kufukuzwa kwenye chama kipindi
hicho. Lakini tulipowakilisha katika
vikao vya chama ilani ilipokelewa
vizuri bila mjadala wowote mkali, na
sisi tukaamini kwamba mapendekezo
yetu ya kuihamisha CHADEMA kiitikadi
na kifalsafa yalikuwa yamepokekewa
vyema.
Hata hivyo juzi nimeshtuka baada ya
kumuona Ali Mfuruki amekaribishwa
kwenye mkutano mkakati wa
CHADEMA uliofanyika huko Kilimanjaro
na kupewa nafasi ya kutoa mada.
Katika mada yake, pamoja na mambo
mengine, Mufuruki alilishambulia sana
Azimio la Arusha na kulaumu kwamba
liliturudisha nyuma. Alishangiliwa vya
kutosha. Viongozi wote wa juu wa
chama, wabunge na wajumbe kadhaa
wa Kamati Kuu walihudhuria mkutano
huo na kumsikiliza vizuri. Ndio kusema
sasa CHADEMA inarudi katika nafasi
yake ya awali kiitikadi na kifalsafa,
yaani mlengo wa kulia. Kwa lugha
nyingine CHADEMA wanarudi katika
asili yao ya ubwanyenye.
Sasa katika kipindi ambapo CCM
hawana mwelekeo wowote kiitikadi na
kifalsafa, na katika mazingira ambapo
chama kikuu cha upinzani wanatamani
ubwanyenye, tunahitaji, tena kama
jambo la dharura, kujenga chama
mbadala. Tunahitaji mbadala kwa
sababu sera za ubwanyenyehaziwezi
kamwe kufanya kazi katika mazingira
ya kwetu zaidi ya kusimika unyonyaji.
Sera za ubwanyenyehata hata huko
magharibi zimeanza kupigwa vita. Sera
za kibwanyenye lazima zipigwe vita
kwa sababu zinagawa watu katika
makundi ya wafanyakazi,
wanaoendelea kumenyeka, na
mabwana na mabibi wakubwa ambao
kazi yao ni kulimbikiza mitaji na faida
bila jasho. Mbaya zaidi wengi wa
mabwana na mabibi wakubwa hawa ni
wakala na makuhadi tu wa
mabwanyenye wakubwa waliopo huko
nje.
Tunahitaji chama ambacho
kitakumbatia na kupigania unyerere
bila aibu. Tunataka chama ambacho
kitasimamia usawa, demokrasia na
uzaleno kama misingi ya sera na
matendo ya viongozi ndani na nje ya
serikali. Tunahitaji chama ambacho
viongozi wake watahubiri uzalendo wa
kweli wa nchi na ambao watakuwa
tayari kuifia nchi yao badala ya kuapa
kufia vyama vyao vya siasa. Tunahitaji
chama ambacho viongozi wake
watatofautisha wakati wa kupanda na
kuvuna. Tunahitaji chama ambacho
kitaunda serikali ndogo lakini yenye
nguvu na kuchukua nafasi yake katika
nyanja muhimu katika kuendesha
uchumi wa nchi na kuimarisha sekta
binafsi inayotambua na kuchukua
wajibu wake katika jamii.
Tunahitaji chama ambacho sera zake
zitatoa fursa kwa sekta binafsi na
asasi za kiraia kufanya kazi sio kwa
hisani ya wanasiasa waliopo
madarakani, bali kwa mujibu wa sheria.
Tunahitaji chama ambacho sera zake
zitawalenga moja kwa moja makundi
maslahi katika jamii, wakiwemo
wanawake, vijana, wazee, walimu,
wakulima wa majembe ya mkono na
pilao, wafanyakazi au wachuuzi.
Kwa kifupi, tunahitaji chama mbadala
kitakachopigania usawa, demokrasia
na uzalendo wa kweli katika nchi.
Kama nilivyosema katika makala yangu
ya wiki jana kujenga chama cha namna
hii hatuhitaji mwongo mmoja kwa
sababu kitajengwa na wananchi
wenyewe kwa sababu kitakuwa ni
chama chao!"
Source: Raia Mwema - Tunahitaji
chama kitakachopigania Unyerere,
kupinga ubwanyenye
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment