-->

SOMA MAKALA MAALUMU YA SHAFFIH DAUDA KUHUSU MUVI YA RAGE PAMOJA NA TIMU YA SIMBA



PART ONE
JUMANNE iliyopita Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are maarufu kama Mzee Kinesi mbele ya waandishi wa habari alitangaza kamati ya utendaji ya klabu hiyo kukubaliana kumsimamisha mwenyekiti Ismail Aden Rage.

Rage alisimamishwa baada ya kamati hiyo kutoridhishwa na utendaji wake lakini kuu ni kukataa kipengele cha marekebisho ya katiba ya klabu hiyo. Mambo yametajwa kumuhusu Rage lakini mengine ni juu ya uuzwaji wa wachezaji Emmanuel Okwi na Mbwana Samatta na sambamba na mkataba wa Azam TV.

Mapinduzi hayo yasiyo rasmi yalitangazwa wakati Rage akiwa Sudan katika vikao vya kamati za bunge za Afrika zinazoshuhulika na hesabu za serikali hivyo wakati uamuzi huo unatangazwa Rage hakuwepo nchini.


PART TWO

Ijumaa ya Novemba 21, 2013 Rage aliwasili nchini kutoka Sudan akiwa na donge moyoni mwake, na kwa bahati nzuri aliwasili salama uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam huku akilakiwa na kundi la mashabiki wachache wa klabu yake.

Apanda ndege moja na Hanspope

Rage aliwasili nchini na ndege ya Shirika la KQ majira ya saa 1:30 akitokea Nairobi ambako aliunganisha ndege akitokea Sudan na kwa bahati alipanda ndege moja na Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspope.

Hanspope alikuwa wa kwanza kutoka uwanjani hapo na kudakwa na waandishi wa habari waliotaka kujua sababu za yeye kuwepo uwanjani pale, na moja kwa moja alijibu kwamba; “Mimi nimetoka Lubumbashi (DR Congo) katika biashara zangu na Rage nimepanda naye ndege moja.”

Aliongeza; “Nimekaa naye jirani kabisa na tumezungumza mengi lakini nimemuhakikishia kwamba nilikuwepo kwenye kikao cha kamati kilichomsimamisha.Msubirini aje hapa mzungumze naye tena msimsubiri hapo maana yeye anatokea VIP.”

Baadaye saa 1:45 Rage alichomoza katika lango la VIP na moja kwa moja alikutana na kundi la mashabiki wa Simba na waandishi wa habari ambao walimuhoji maswali lukuki lakini alisimamia msimamo wa kuozungumza hadi kesho yake (jana jumamosi).

“Nashukuru nimefika salama na napenda kuwaambia kwamba mimi ndiye mwenyekiti wa Simba hakuna mtu mwingine mwenye cheo hicho,” alipoulizwa zaidi kuhusu uamuzi wake juu ya maamuzi hayo ya kamati, Rage alisema; “Unajua rafiki yangu Zitto Kabwe amepata matatizo ya kusimamishwa katika chama chake kwa hiyo sipo katika mood ya kujibu maswali mengi.”

Rage akasema; “Kesho Jumamosi nitazungumza na waandishi saa saba kamili.”

Aondoka na kamsafara zake

Baada ya kauli hiyo, Rage aliondoka uwanjani hapo na gari aina ya Toyota Granvia lenye namba za usajili T 300 CPR. Gari hilo lilifuatiwa na mabasi matatu yenye uwezo wa kuchukua abiria wasiozidi 25 ambalo la kwanza lilikuwa na namba za T 885 BNT, T 208 BFM na lingine lenye namba T 549 BZQ.

Msafara huo wa Rage ulienda hadi makao makuu ya klabu hiyo ambapo ulisimama kwa muda kisha ukaondoka klabuni hapo huku kila mmoja akidhani kesho Rage atatoa neno.

PART THREE

Huku umma ukiwa na shauku ya kufahamu kitakachozungumzwa na Rage, asubuhi ya Jumamosi ya jana, likatoka tangazo kwamba, Rage hasingeweza kuzungumza siku hiyo na badala yake atafanya hivyo leo Jumapili.

Sababu kubwa ya Rage kutozungumza jana ilisemwa ni yeye kupata nafasi ya kwenda TFF kupeleka barua yake ya kuelezea mchakato wake wa kusimamishwa ikiwa ni baada ya Mzee Kinesi kupeleka barua ya kumsimamisha Rage.


PART FOUR

Mungu si Athuman, TFF ikaona Rage ana hoja na moja kwa moja ikamuagiza aitishe mkutano wa wanachama ndani ya siku 14 ili kumaliza tofauti za kiungozi zilizopo.

TFFilitoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa mgogoro katika klabu baada ya kupokea barua mbili; moja kutoka Kamati ya Utendaji ikielezea kumsimamisha uongozi Rage, na nyingine kutoka kwa Mwenyekiti huyo ikielezea kutotambua kusimamishwa huko.

Uamuzi wa TFF ulifanywa kwa kuzingatia Ibara ya 1(6) ya Katiba ya Simba inayosema: “Simba Sports Club ni mwanachama wa TFF, itaheshimu Katiba, kanuni, maagizo na uamuzi wa TFF na FIFA, na kuhakikisha kuwa zinaheshimiwa na wanachama wake.”

TFF ikasema itatuma wawakilishi wake katika mkutano huo, na kumuagiza Mwenyekiti wa Simba kuhakikisha wanachama wote wenye hoja wanapata fursa ya kusikilizwa.

PART FIVE

Leo hii Rage amesema hawezi kuitisha mkutano mkuu wa dharura kama alivyoelekezwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuwa shirikisho hilo halina mamlaka ya kufanya hivyo.

Rage alisema TFF haiwezi kumlazimisha kufanya hivyo na ikiendelea kumlazimisha kufanya hivyo atajiuzulu nafasi yake kwani amechoka kuona anaonewa kila siku.

Kina Mzee Kinesi walikaa kikao cha harusi

“Watu walionisimamisha wanasema ni maamuzi ya kamati ya utendaji, hii siyo kweli kile hakikuwa kikao cha kamati ya utendaji bali ni kikao cha kawaida tu kama kikao cha harusi.

“Katiba ya Simba ibara ya 28 (1) kuanzia a, b, c mpaka d inasema wazi kwamba, maana ya kamati ya utendaji ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe saba. Na kamawakitaka kukaa, mwenyekiti ndiye mwenye jukumu la kuitisha kikao au makamu mwenyekiti kwa ridhaa ya mwenyekiti kama akiona kuna ulazima wa kufanya hivyo,” alisema Rage.

Rage alisema katiba ya Simba inamtaka mwenyekiti kuitisha vikao vinne kwa mwaka, yaani kimoja kila baada ya miezi mitatu.”Sasa mimi nimeshaitisha vikao 12 ndani ya mwaka huu,” alihoji Rage. 

Aidindia TFF, aishangaa kuwatambua kina Kinesi

Rage anasema alipeleka barua yake TFF kuelezea uhuni huu uliofanywa na hao watu, lakini anashangaa kwa nini TFF hawakutoa tamko lolote la kulaani kinachoitwa mapinduzi na badala yake wanamlazimisha kuitisha mkutano.

“Katika katiba ya Simba, Ibara ya 22 inaelezea kuhusu mkutano mkuu, haya si maneno yangu lakini nanukuu hapa, inasema mwenye wajibu wa kufanya hivyo ni mwenyekiti kwa kushirikiana na kamati ya utendaji kama anaona inafaa. Sasa hili la maelekezo ya TFF linatoka wapi?,” alihoji Rage.

Adai kuna mbaya wake TFF, wakimzingua anajiuzulu

Rage anasema kuna kiongozi mmoja yupo ndani ya TFF ambaye zamani alikuwepo Simba na akashindwa akaondoka zake lakini sasa ndiye anayemchafua ili tu aweze kurejea Simba lakini yeye anamuachia mungu.

“Kuna kiongozi mmoja aliyekuwa Simba na sasa yupo ndani ya kamati ya utendaji ya TFF, huyu ananiandama na kunichafua kila siku. Niliwapelekea TFF barua ya mambo yote haya na ilipaswa kamati ya maadili ipitie lakini badala yake kamati ya utendaji ndiyo iliyofanya kazi hiyo, hakuna kitu kama hicho. Sasa wakiendelea kulazimisha mkutano mimi nitajiuzulu.”

“Tazama mfano huu, wakati uchaguzi wa TFF ulipoingia katika mgogoro kwa baadhi ya wagombea, Fifa ilielekeza uchaguzi huo ufanyike baadaye lakini si kwa kuipangia TFF kama wanavyoniambia mimi,” alisema Rage na kuongeza.


Amuingiza vitani Wambura, ampa ulaji Malkia wa Nyuki

Rage kabla hajamaliza mkutano wake na waandishi wa habari alitangaza kumteua Michael Wambura kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba na huku akimtaja Rahma Al Kharoos kuwa mjumbe wa baraza la wadhamini la Simba.

“Namtangaza Michael Wambura kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba, huyu anachukua nafasi ya malkia wa nyuki (Al Kharoos) aliyeniomba kutolewa katika kamati hiyo kutokana na kubanwa na kazi zake.

“Nimemuomba malkia wa nyuki aingie katika baraza la wadhamini na kuanzia sasa yeye atakuwa mmoja wa wajumbe wa baraza la udhamini na jina lake nitalipeleka likathibitishwe na mkutano mkuu hapo baadaye,” alisema Rage.

Kwa uteuzi huo ina maana Rage sasa atakuwa na mjumbe mmoja anayemuunga mkono ambaye ni Wambura. Wambura huyu anaelezwa kutowakubali Friends of Simba kundi linaloiongoza Simba kwa sasa.

Awaacha waandishi bila kujibu maswali, aondoka nchini

Muda mfupi baada ya mkutano huo na waandishi wa habari, Rage aligeuka mbogo kwa kukataa kujibu maswali ya waandishi wa habari huku akisema anayetaka kuandika habari hiyo naandike na asiyetaka aachane nayo.

“Sitaki maswali hapa, anayetaka kuandika aende kuandika na asiyetaka aache, wengi humu mnatumiwa na hawa watu, sasa ni kipi mtakachoniuliza?, sitaki swali tuondoke,” alisema Rage huku akinyanyuka.

PART SIX

Mtandao huu uliwasiliana na TFF ambapo kaimu katibu mkuu wake ndiye aliyepatikana na aliposomewa maamuzi ya Rage, akasema hakuna tatizo kwa Kamati ya Utendaji ya TFF kutoa uamuzi huo hivyo si kweli kwamba hawakuwa sahihi kutoa maelekezo hayo kwa Rage.

Wambura alisisitiza kwamba, wanasubiri siku 14 ziishe halafu wachukue uamuzi endapo mkutano mkuu hautafanyika ndani ya Simba.

“Sisi tunangoja siku 14 zipite halafu utaona tunafanya kitu gani leo  ndiyo kwanza siku ya pili, yeye kama amesema hivyo wacha tungoje siku 14 ziishe halafu tutakuwa na uamuzi wetu,” alisema Wambura.

USIKOSE PART SEVEN BAADA YA SIKU 12 zijazo
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment