“Ameingia rasmi katika orodha ya wanasiasa wanaofaa kupuuzwa
na kutopewa nafasi ya uongozi. Ile kauli ya Mohammed (Eddy) Riyami, kada
aliyeasi CCM, ya wananchi kuwafuta viongozi wasioitakia mema Zanzibar
na watu wake, imethibiti.”
Na Jabir Idrissa
NILIPONUKUU maneno aliyoniambia Samwel John Sitta kupitia simu ya
mkononi (rudia makala iliyopita), sikujua bwanamkubwa huyu ana kiburi
cha kupindukia mpaka.
Mshangao niliopata kuhusu hulka yake hiyo baada ya kumsikiliza
Septemba 2014, haujapungua uzito. Sikuwahi kumjua kwa sura yake halisi.
Na tatizo zaidi linakuja ninapojiuliza hivi mtu huyu mwenye hadhi
kubwa kisiasa kutokana na kupata vyeo vikubwa serikalini, anajisikiaje
anapoporomosha maneno ya chuki na ubabe?
Najisumbua. Mtu na hulka yake inafanana na mbwa na bwana wake – wanapatana na kurandana nyakati zote, iwe jua iwe mvua.
Ni hakika kabisa Sitta ana hulka ya kiburi na jeuri hata pale
anapojua fika anaowaonesha sifa hizo mbaya ni watu wanaofikiri sawasawa
na kwa kiwango.
Sasa amejifunua zaidi na amejikaanga kwa mafuta yake. Ni kama pweza –
kujikunja kadiri anavyoguswa na uzito wa moto huku akizidi kuteketea.
Pweza, samaki mtamu na ambaye mchuzi wake una rutuba muhimu kwa ujenzi
wa mwili wa mwanadamu, huangamia kila anapojipinda akifikiri anapambana
na moto anapochomwa.
Ajabu Sitta anavyojifanya msahaulifu. Amesahau kishindo alichopata
ukumbi wa Sekondari ya Haile Sellasie, mjini Zanzibar, mwaka 2011,
aliposhuhudia upinzani wa Wazanzibari kuhusu muswada wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba aliokwenda nao kwa lengo la kuuelimisha.
Hakustiriwa chembe, bali alioneshwa waziwazi kuwa Wazanzibari walio
wengi hawataki kuburuzwa na kufanywa kama vile watu wasiojitambua au
watoto wasioelewa historia ya nchi yao, mila na desturi yao, na kwa
jumla, utamaduni wao.
Muswada aliopeleka ulichanwa mbele yake na ujumbe wake akiwepo Samia
Suluhu Hassan ambaye alikuja kuwa makamu mwenyekiti wake katika Bunge
Maalum la Katiba.
Sitta alitakiwa kurudi kwa waliomtuma Serikali ya Jamhuri ya Muungano
na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichochuja na kukataliwa Zanzibar, na
sasa Tanganyika ambako kimekuwa kikiamini kingali na mvuto.
Nilisema Sitta hastahili kuheshimiwa wala kufikiriwa kuwa kiongozi na
kutarajia kura za Wazanzibari. Nikamweka kundi na Bernard Kamilius
Membe, ambao wanapatana.
Sitta ametangazia vita Wazanzibari wenye asili ya Pemba. Ameonya
wasimchezee na kwa wale wanaojitia kupinga Muungano, anasema, ole wao,
watakiona cha mtemakuni.
Amewaweka wananchi hao kundi moja na viongozi wa Chama cha Wananchi
(CUF) akisema atawashughulikia kwa nguvu zake zote atakapokuwa Rais wa
Tanzania. Swadakta. Ujumbe wake umewafika Wazanzibari.
Wazanzibari wanaoupinga muungano wa mfumo wa serikali mbili
unaolelewa na CCM, si Wapemba tu, hata Unguja. Wanataka Muungano wa
serikali tatu, tena wa kuipa Zanzibar mamlaka yake kamili.
Wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipokuwa ikipita majimboni
kukusanya maoni ya Wazanzibari kuhusu wanavyotaka Katiba mpya ya Jamhuri
ya Muungano iwe, walijadili kwa upana mustakbali wa Muungano. Walitaka
mabadiliko ya mfumo, na ikibidi kama hautabadilishwa, basi walihiyari
uvunjiliwe mbali.
Hivyo basi, kwa upinzani wa muungano wa mfumo unaolelewa na CCM,
Sitta na wenzake waliokusudia kuwavurumishia mizinga na maji ya kuwasha
Wazanzibari, watambue si Wapemba tu watakaokutana nao.
Sitta amedhihirisha asivyo muungwana bali mwanasiasa jeuri na mpenda
uongozi wa mabavu. Anapenda kulazimisha watu kutaka atakalo na atakavyo;
kuamini anavyoamini na anavyofikiria. Hataki mawazo yasiyoendana na
yake. Mhafidhina.
Ameapa atavunja ngome ya CUF kisiwani Pemba. Huyu mwanasiasa
anayetafuta kupewa dhamana ya kuongoza jamhuri ambayo Zanzibar ni sehemu
muhimu, anachekesha. Unavunjaje ngome ya CUF iliko asili yake?
Sitta amefika Zanzibar kutafuta wanachama wa CCM wa kumdhamini katika
fomu zake za kuomba ateuliwe kugombea wadhifa wa urais wa Tanzania
ifikapo Oktoba 2015.
Anafika Pemba ambako ni sharti kwa kila muombaji wa uteuzi huo kufika
na kupata wadhamini, kati ya wale 450 wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni
za chama chao. Maneno yake hayo ndiyo ujumbe anaowaachia wananchi wa
Pemba. Na kwa mantiki ya mjadala huu, ndio ujumbe anaowaachia
Wazanzibari – “ole wao, nitawaonesha cha mtemakuni.”
Ina maana Sitta amedhamiria kuongoza kwa chuki na hasira dhidi ya
wananchi wasioukubali Muungano kwa mfumo unaolelewa na kung’ang’anizwa
na CCM, kama vile kilivyofanikiwa kuubakisha mfumo huo kwenye Katiba
Inayopendekezwa, iliyopitishwa kiunajimu na Bunge Maalum la Katiba
aliloliongoza.
Alikuwa Sitta aliyeapa kutimiza kura za kufikia theluthi mbili ya
mahitaji ya kuidhinisha katiba kuwa imeridhiwa na bunge hilo. Kweli
alifanikiwa kufikisha matakwa ya sheria, lakini kila mjumbe wa bunge na
yeye mwenyewe wanajua kwa uhalisia, ghushi iliyotumika. Na ajuwe iko
siku ukweli wa kilichotokea utawekwa wazi na yeye na wenzake kuchukuliwa
hatua.
Sitta amewakosea Wazanzibari na ameikosea nchi yao. Ameidharau
historia ya Zanzibar na utamaduni wa Wazanzibari kupenda ukweli na
utamaduni wao. Ameandika historia ya kishetani isiyosahaulika na
historia.
Aliowatuma wamfanyie kazi ya kishetani wanasema walichokitenda.
Wanasema walichokipata. Hata kama hawasemi hadharani, wanasema na nyoyo
zao. Wanasema. Kwa kuwa walichokifanya baada ya kutumwa kukifanya chini
ya maelekezo yake Sitta, ni kibaya kisichokubalika kisheria na
kimaadili, dhamira zao zinawaumiza hata kama wanapotezea.
Sitta mwenyewe hawezi kujiangalia sawasawa kama mtu muadilifu.
Amejifutia ile dhana yake ya utendaji wa kiwango na kasi. Haikustahili
kasi na kiwango katika kupanga maovu. Hata kidogo.
Dhana hii ilipaswa na inapaswa kutumika kutengeneza kitu kizuri
kinachosaidia kuandika historia ya maendeleo ya kweli ya mwanadamu na
siyo uchafu na uhalifu. Hata chembe.
Sitta amejibiwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad
ambaye anasubiri tu muda achukue fomu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
(ZEC) kuwania tena kiti cha urais wa Zanzibar.
Sitta anamjua Maalim Seif. Anakumbuka majibu yake alipokwenda
kumshawishi asaliti Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) eti kwa
kumuahidi cheo na fedha. Masikini Sitta ameshindwa kusoma alama za
nyakati.
Alikubali vipi kubeba mzigo mchafu na kumfikia mwanasiasa
anayefahamika alivyo muungwana, muadilifu, muaminifu na makini kiuongozi
na kidhamira? Hajui Maalim Seif amechukua ahadi kuwa na Wazanzibari
itakavyokuwa.
Kwa kuwa Sitta hatarajiwi kupika wala kupakua yanapokuja masuala
wanayoyaamini Wazanzibari kuwa ni haki yao, ajue alijiumbua na kuumbuka
mwenyewe. Amejishusha.
Kilicho kibaya zaidi ni kuendelea kujishusha kwa kujitwisha mfupa
uliomshinda fisi – kuyabadili matumaini ya Wazanzibari kuhusu kupata
mamlaka kamili. Tofauti na anavyoeneza chuki za kidini na usultani.
Walishindwa waliomtangulia, atashindwa binafsi na CCM anayoiabudu
imteue.
IMENUKULIWA KUTOKA:ZANZIBAR YETU
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment